HakiElimu, Save the Children, Msichana Initiative, TCRF, CiC, Children Dignity Forum, Shule Direct kwa pamoja na asasi zingine za kiraia ambazo ni vinara wa upingaji ukatili kwa watoto ikiwemo adhabu za kikatili shuleni, tumesikitishwa na taarifa za kifo cha mwanafunzi wa kidato cha pili, Mhoja Maduhu, kutoka Shule ya Sekondari Mwasamba, Kata ya Lutubiga, Wilaya ya Busega, Mkoani Simiyu, ambacho kinatajwa kutokana na adhabu ya viboko iliyotolewa na Mwalimu wake Februari 26, Mwaka 2025. Kwa pamoja, tunatoa pole sana kwa familia, ndugu na taifa kwa ujumla kwa kifo cha mwanafunzi huyu.
Ndugu wanahabari: Tunaamini pia mmepitia na kusoma taarifa za kifo hiki kupitia vyombo mbalimbali vya habari ambazo zinadai, mtoto huyu alifariki kutokana na majeraha yaliyotokana na adhabu ya viboko 10 kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani. Vipimo vya kitabibu vilivyofanywa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando vimebaini kuwa damu ilivujia kwenye ubongo wa marehemu, hali inayoashiria madhara makubwa aliyoyapata kutokana na kipigo hicho.
Tunalaani na kukemea tukio hili ambalo sio tu linakiuka miongozo ya utolewaji wa adhabu za viboko shuleni, lakini pia linaendeleza vitendo vya ukatili kwa watoto shuleni ambavyo kwa sehemu kubwa vimekuwa vikififisha mazingira salama ya kujifunza na utolewaji wa elimu hapa nchini.
Ndugu wanahabari: Tukio hili linafanana sana na tukio la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius Mwaka 2018 aliyekuwa anasoma shule ya Msingi Kibeta, Manispaa ya Bukoba ambaye alifariki kutokana na adhabu ya viboko toka kwa mwalimu wake. Pamoja na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa walimu husika, tunasikitika kuona matukio ya namna hii bado yanajitokeza katika jamii na shule zetu.
Utafiti wa HakiElimu wa Mwaka 2020 unaonyesha kuwa kuna matukio mengi ya vitendo vya ukatili mashuleni. Takribani asilimia 87.9 ya wanafunzi waliripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili, ambapo asilimia 90 ya hao wanafunzi waliripoti kuwa ukatili huo waliofanyiwa ulitokana na adhabu za viboko toka kwa walimu wao. Lakini pia asilimia 89 ya wanafunzi walisema ukatili wa kimwili unafanyika shuleni ilihali asilimia 10 walisema unafanyika nyumbani.
Ndugu wanahabari: Tunaamini, kujirudia kwa matukio kama haya kunatokana na kuwepo kwa mianya ya kisheria, na kitamaduni inayoruhusu utolewaji wa adhabu hizi mashuleni. Tunafahamu kuwa upo mwongozo wa utolewaji wa adhabu za viboko shuleni ambao unataka adhabu hii kutolewa na Mkuu wa shule au Mwalimu aliyekasimishwa kwa maandishi, na kuwa idadi ya viboko visizidi vinne. Lakini tumeshuhudia mwendelezo wa ukiukwaji na kutofuatwa kwa miongozo hii kwa kiasi kikubwa. Hii ndiyo sababu, mashirika ambayo ni vinara wa upingaji wa adhabu ya viboko shuleni – tunapinga uwepo wa adhabu ya viboko mashuleni kwa namna yoyote ile.
Wito wetu siku zote umeitaka serikali kuondoa kabisa adhabu za viboko shuleni na kuufuta Mwongozo na Kanuni zozote ambazo zinaruhusu utolewaji wa adhabu za viboko kwa kuwa utekelezaji wake umekuwa mgumu na hivyo kupelekea ukiukwaji mkubwa wa haki za Watoto shuleni na wakati mwingine maafa kama haya kutokea.
Kutokana na Mwongozo wa Elimu wa 2002 juu ya Adhabu za Viboko (The Education Corporal Punishment Regulations 2002), Mwalimu mkuu ndiye anaruhusiwa kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha jukumu hilo kwa maandishi kwa mwalimu mwingine. Mwongozo huu umepewa nguvu na sheria ya Elimu ya mwaka 1978 mabadiliko ya 2002 ambapo chini ya kipengele cha 60 kinaruhusu utolewaji wa adhabu mbalimbali kwa ajili ya kuhimiza nidhamu kwa wanafunzi.
Kutokana na matukio haya, tunatoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za kukomesha kabisa matumizi ya adhabu za viboko shuleni na kuhimiza adhabu chanya/adhabu mbadala ambazo sio za kikatili ambazo zitahimiza nidhamu kwa wanafunzi. Tunatoa rai kwa mambo yafuatayo kufanyika ili kukomesha ukatili kwa wanafunzi na kuzifanya shule ziwe salama.
Kuondoa Mwongozo wa elimu wa 2002 juu ya adhabu za viboko (The Education Corporal Punishment Regulations 2002) na kuandaa mwongozo mwingine wa adhabu chanya/adhabu mbadala ambao utachagiza utolewaji wa adhabu zisizo na kikatili kwa wanafunzi. Ushahidi wa kitafiti wa HakiElimu uliofanyika katika shule 8 za majaribio kuhimiza matumizi ya adhabu Chanya, umeonyesha kuwa asilimia 98 ya wanafunzi wanajihisi kuwa salama kwa sababu walimu hawatumii adhabu za viboko. Serikali inaweza kutumia ushahidi huu kama funzo kuwa matumizi ya adhabu chanya yanawezekana katika kuhimiza nidhamu kwa wanafunzi bila kuwafanyia ukatili.
Serikali kutumia fursa ya mchakato wa mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 unaoendelea hivi sasa kuweka vipengele vya kuzuia matumizi ya viboko shuleni na adhabu zingine zinazotoa mwanya kwa walimu kufanya ukatili kwa wanafunzi. Kuweka sheria ya kupiga marufuku viboko itasaidia kuzuia walimu kutumia adhabu hizi, na hivyo kupunguza na kuondoa kabisa ukatili kwa wanafunzi shuleni.
Serikali kuweka mpango wa utekelezaji ahadi iliyoiweka katika Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa Dunia kuhusu kutokomeza ukatili dhidi ya watoto uliofanyika Bogotá, Colombia mnamo Novemba 2024, wa kuanzisha Madawati ya Ulinzi wa Watoto katika shule zote 26,659 ifikapo mwaka 2029. Madawati haya yatatoa mfumo rasmi wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya watoto wanaokumbwa na ukatili wa aina mbalimbali shuleni, ikiwa ni pamoja na vipigo, unyanyasaji wa kijinsia, na manyanyaso ya kisaikolojia.
Limetolewa na Mashirika Vinara wa Upingaji wa adhabu za kikatili Shuleni Leo Tarehe 6/03/2025.
1. Children Dignity Forum
2. TCRF
3. Save the Children
4. Msichana Initiative
5. Children in Cross Fire
6. Shule Direct
7. HakiElimu
Comments